KOCHA GENK AMTULIZA SAMATTA
.
Kocha wa KRC Genk, Wouter Vrancken amewataka wachezaji wake kujitoa haswa kwenye mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Royal Antwerp bila kuzingatia matokeo ya mchezo mwingine wa mchujo kati ya Royale Union Saint-Gilloise na Club Brugge kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro’.
.
Raundi ya mwisho kwenye mchujo wa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji itachezwa kesho, Jumapili, huku presha ikipanda na kushuka kwa mashabiki wa KRC Genk anayoichezea nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, Royal Antwerp na Royale Union Saint-Gilloise ambazo zipo kwenye nafasi ya kwanza hadi tatu.
.
Vrancken alisema hayo ili wachezaji wake waelekeze fikra na mawazo yao kwenye mchezo dhidi ya Royal Antwerp. ”Ni mbaya wakati unacheza kuwa na mawazo ya matokeo ya mchezo mwingine hiyo ni mbaya inaweza kupunguza ufanisi wao.”
.
“Tunatakiwa kufanya vizuri kwanza halafu hayo mambo mengine yatafuata baadae. Tunataka kuwapa kilicho bora mashabiki wetu ambao wamekuwa pamoja na sisi tangu mwanzoni mwa msimu,” alisema kocha huyo ambaye enzi zake alikuwa kiungo mkata umeme.
.
Katika mchezo huo wa mwisho wa msimu, nahodha wa Taifa Stars, Samatta ndiye atakayekuwa na jukumu la kuongoza mashambulizi ya KRC Genk ambayo ipo nafasi ya tatu.

Comments
Post a Comment