SIMBA, YANGA MWENDO WA NOTI .
.
Simba imeng’olewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, lakini taarifa njema kwao ni kule kuongezwa mkwanja ikijihakikisha kuvuna Dola 900,000 (zaidi ya Sh 2.1 bilioni) baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza mzigo wa fedha za zawadi kwa michuano ya msimu huu.
.
Ongezeko hilo la fedha halijainufaisha Simba tu, bali hadi watani wao, Yanga ambao wametinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwani hadi sasa ina uhakika wa kuvuta Dola 1 milioni (Sh 2.35 bilioni, badala ya 1.8 bilioni zilizokuwa kwenye kiwango cha zawadi cha awali ikimaliza ya pili.
.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi jioni kwenye mtandao wa CAF, zawadi za msimu huu zimeboreshwa kwa asilimia 40 ikiwa ni utekelezaji wa ratifa zilizowahi kutolewa na Rais wa Shirikisho hilo, Dk Patrice Motsepe mapema mwaka huu juu ya ongezeko hilo.
.
Kwa mujibu wa viwango vya sasa vya zawadi hizo kwa Ligi ya Mabingwa, Bingwa anazoa Dola 4 milioni (zaidi ya Sh 9.4 bilioni), huku anayemaliza wa pili atanyakua Dola 2 milioni (zaidi ya Sh 4.7 bilioni) na zile zilizoingia nusu fainali zinakomba Dola 1.2 milioni ( zaidi ya Sh 2.8 bilioni) na zile za robo ambayo Simba nayo ipo hapo ni Dola 900,000 ( zaidi ya Sh 2.1 bilioni).

Comments
Post a Comment